Mtandao huu hivi karibuni ulifanya mahojiano na Katibu Mkuu wa CUF
ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa, Maalim Seif Sharif Hamadi nyumbani kwake Ilala jijini Dar es
Salaam. Ungana nasi katika mahojiano hayo ufahamu mengi aliyoyasema:
Swali: Suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) lipo kwenye katiba ya Zanzibar au yalikuwa ni makubaliano ya mdomo?
Jibu: Serikali ya Umoja wa Katiba (SUK) imo ndani ya katiba, isipokuwa
hii ya sasa hivi ya Dk. Ali Mohammed Shein haipo, tena basi sisi
hatuitambui kwa sababu imepora ushindi wetu.
Katiba ya Zanzibar inasema wazi kwamba Muundo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa kwa mujibu wa Marekebisho ya 10 ya Katiba ni kuwa na Rais
Mtendaji, Makamu wa Kwanza wa Rais atakayeteuliwa na rais baada ya
kushauriana na chama cha siasa kilicho pata nafasi ya pili katika
matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais, makamu wa pili wa rais
atakayeteuliwa na rais kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka katika chama cha siasa anachotoka rais.
Pia, rais kwa kushauriana na makamu wote wawili atateua mawaziri kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuzingatia uwiano wa
viti vya majimbo kwa vyama vya siasa vilivyomo ndani ya Baraza la
Wawakilishi lakini serikali hii ya Shein imekiuka hayo yote kwani hakuna
chama kilichokidhi matakwa hayo ya katiba. Swali: Baada ya nyinyi yaani
wewe na Rais Amani Abeid Karume kukubaliana ni nini kilifuata? Jibu:
Pamoja na kuunda jopo la watu sita, bado tukaona suala hili lipelekwe
kwenye Baraza la Wawakilishi ili lipitishwe kisheria.
Kule lilipelekwa kama hoja na Mheshimiwa Abubakar Khamisi Bakary
likajadiliwa na likapitishwa. Lakini hata hivyo, ikaonekana lazima
lipelekwe kwa wananchi likapigiwe kura.
Bunge likaunda kamati ya watu sita kusimamia jambo hilo na watu hao ni
Ali Mzee Ali (CCM), Abubakar Khamisi Bakary (CUF), Ali Abdallah Ali
(CCM), Haji Omar Kheri (CUF), Nassor Ahmed Mzrui (CUF) na Zakiya Omar
Juma (CCM), walifanya kazi nzuri sana wananchi wa Zanzibar walipiga kura
ya maoni siku ya Jumamosi Julai 31, 2010.
Kura hiyo ilikuwa na lengo la kutafuta ridhaa ya wananchi katika kuamua
iwapo wanalikubali wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010.( Matokeo hayo yalitoa
ushindi wa kura za NDIO kwa asilimia 66.40% dhidi ya kura za HAPANA
asilimia 33.90%)
Swali: Kuna madai kuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume ni rafi ki
yako na mfuasi wa CUF, je kuna ukweli wowote katika hili?
Jibu: Siyo kweli kwamba Rais Mstaafu Amani Karume ni mfuasi wa Cuf
isipokuwa siri iliyopo ni kweli kwamba Karume anapenda amani na
maendeleo ya watu wa Zanzibar kwa sababu ndiye tuliyejadiliana naye na
kukubaliana kuundwa kwa serikali ya kitaifa tukaacha itikadi zetu. Hii
siri wengi hawajui.
Swali: Kama Karume siyo CUF ilikuwaje hadi mkakubaliana kuunda serikali ya kitaifa?
Jibu: Siku moja tukiwa msibani tulionana na mzee Hassani Nassoro Moyo,
tukajadili kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, akasema kwa nini tusikae
meza moja kuondoa kasoro zetu za kisiasa ili nchi isonge mbele?
Nilimwambia nitakwenda kwake kuonana naye. Kweli nilikwenda na
tukazungumza. Akasema atakwenda
kuonana na Rais Amani Karume ampe ujumbe huo, alikwenda na baada ya siku
chache akaniambia rais amekubaliana na wazo hilo hivyo atapanga siku
mkutane. Kweli siku moja nikapigiwa simu kualikwa na rais ikulu,
nikaenda na kujadiliana kuhusu serikali ya kitaifa. Tulikubaliana tuunde
kamati ya watu sita, watatu wa CCM na watatu wa CUF ili wapate njia ya
kufanya.
Swali: Kwa mtazamo wa CCM, Maalim hawataki uwe rais wa Zanzibar wakidai
eti unataka kuwarudisha Waarabu. Unaweza kutoa ufafanuzi wa hofu hii ya
chama tawala?
Jibu: Kwanza ni kweli kwamba CCM hawataki mimi niwe rais wa Zanzibar kwa
sababu nawajua, wana hofu kwamba nikiwa rais nitalipa kisasi kutokana
na mambo mabaya waliyonifanyia lakini nasema kwa dhati kutoka moyoni
kwangu kwamba hilo siwezi kulifanya.
Mimi nawaambia ninachoangalia ni maendeleo ya watu wa Zanzibar, basi,
hofu ya kisasi waondoe. Lakini hata hicho kinachosemwa kwamba
nitawarudisha Waarabu, ni Mwarabu gani atakayerejea Zanzibar? Hizo ni
propaganda tu za CCM. Historia ya visiwa vyote duniani vina watu
mchanganyiko, hata ukienda Mauritius, Seycheles, Comoro ni hivyo.
Swali: Wewe unamfahamu zaidi Profesa Lipumba kuliko wengi wanavyofi kiri,
unaweza kutueleza ni nini hasa kimembadili Lipumba kuwa alivyo?
Jibu: Profesa Ibrahimu Lipumba nimeanza kumfahamu tukiwa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam miaka mingi sana iliyopita, hivyo ni kweli namfahamu sana.
Tukiwa chuo tulikuwa kwenye umoja wa dini ya Kiislamu pale chuoni.
Kwenye harakati za kisiasa ni mimi ndiye niliyependekeza aitwe atusaidie
kwanza kama mshauri wa chama, baadaye akawa mwenyekiti. Sasa ukiniuliza
kwa nini amebadilika, siwezi kukupa jibu, hilo anatakiwa alijibu yeye
mwenyewe.
Swali: Huoni kwamba mgogoro wenu umesababisha chama kugawanyika?
Jibu: Chama hakikugawanyika, mgogoro uliopo umetengenezwa na msajili wa
vyama kwa sababu Lipumba amekataliwa na vikao halali vya chama na siyo
na Maalim Seif, kwenye mkutano mkuu wa CUF una wajumbe kama 475
waliomkataa na kusema afukuzwe uanachama ni wengi na waliosema
asifukuzwe ni 14 tu.
Swali: Kwa mara ya kwanza Cuf ilipata wabunge wengi Bara katika
uchaguzi, unadhani hii ni sababu ya kukubalika kwa chama hicho upande wa
Bara au kilisaidiwa zaidi na muungano wa Ukawa?
Jibu: Vyote viwili, chama kimekubalika lakini Ukawa umesaidia vyama
vyote vilivyoungana. Huko nyuma tulikuwa tukiwashinda CCM lakini sisi
kura zetu zilikuwa zikigawanywa, sasa Ukawa umesaidia CUF na Chadema na
hata NCCR ndiyo maana tumepata wabunge, uchaguzi ujao tutapata wabunge
wengi zaidi.
Itaendelea...
Subscribe by Email
Follow Updates Articles from This Blog via Email

No Comments