G Nako ni msanii ambaye sauti yake ni bidhaa ambayo inauzika kirahisi katika soko la muziki wa Bongo Fleva kwa sasa, ameweza kuuza bidhaa hiyo vema tangu kipindi cha Nako 2 Nako Soldiers, hadi sasa Weusi.

Ingawa inafahamika chimbuko la G Nako ni katika muziki wa hip hop/rap, ila amekuwa hatabiriki kwa namna anavyodilisha flow kila mara hadi unaweza kujiuliza yeye binafsi anaamini katika aina ipi ya muziki. Jamaa anarap na kuimba kwa wakati mmoja, uzuri ni kwamba anamubu vyote kwa wakati mmoja, hivyo anajichotea mashabiki wa pande zote mbili kitu ambacho wasanii wengi kimewashinda.
Ndiyo kimewashinda, unaweza kumuona msanii anafanya vizuri katika rap ila anapoamua kubadilika na kuanza kuimba anashindwa, yaani hafanyi vizuri jambo ambalo huweza kumfanya kupoteza mashabiki wake wa awali.
Huu mchezo wa pande zote mbili muachie G Nako, ndio maana utamuona akifanya vizuri akiwa na Jux na Bela, wakati huo huo anafunika akiwa na Mwana FA, Country Boy au Izzo Bizness, yaani jamaa ni wa ngumu nyeusi na laini fulani.
Tumchambue G Nako kwa kuangalia kule alipofanya vizuri zaidi katika rap na kuimba, tuanze na rap. Wasanii wengi wa hip hop wanapomshirikisha G Nako hupenda aimbe chorus katika ngoma zao, na stori zilizopo mtaani ni kwamba chorus za G Nako hazijawahi kumuacha mtu salama, weka nukta hapo.
Wasanii hawa wa rap au hip hop, hufanya hivi ili kuleta utofauti kwani kinachotakiwa ni ile sauti ya G Nako yenye kuamsha ‘mizuka’. Izzo Biziness, Mwana FA, Stereo na Country Boy ni mashahidi wa hilo.
Izzo Biziness alimshrikisha G Nako katika wimbo wake ‘Shem Lake’ ambao Mwana FA alipata nafasi ya kudondosha verse moja ya nguvu. Kabla ya ngoma hiyo Mwana FA alikuwa ameshafanya wimbo na G Nako uliofahamika kama ‘Mfalme’.
Kwa upande wa Stereo na Country Boy, hawa ni marapa ambao tunaweza kuuweka muziki wao sehemu moja katika kiwango cha ushindani, kama wanazidiana si kwa kiwango kikubwa.
Stereo ambaye kwa sasa anafanya vizuri na wimbo wake ‘Mpe Habari’ aliomshirikisha Rich Mavoko, alimpa shavu G Nako kwenye wimbo wake uliokwenda kwa jina la ‘Sana’ chini prodyuza Rash Don wa Kiri Records.
Kwa upande wa Country Boy ameshafanya kazi mbili na G Nako, hii inamaanisha kufanya kazi na G Nako ni biashara nzuri na ambayo inalipa. Wimbo wa kwanza ulifahamika kama Watch Me, kisha kufutiwa na wimbo uitwao Mtaa kwa Mtaa’.
Upande wa pili
Pia wasanii wa kuimba katika miondoko tofauti tofauti kama zuku na Rnb nao hawakuwa mbali kuinasa sauti ya G Nako katika ngoma zao. Hawa walimtafuta G Nako ili aje kurap katika nyimbo zao, lakini lile kundi la kwanza (hip hop/rap) ilikuwa ni kinyume na hao.
Hapa ndipo unakuja utamu na ubabe wa G Nako katika game, na sababu ya mimi kuhoji ‘Imani ya G Nako ni ipi katika muziki huu?.
Rama Dee na Damian Soul, ni miongoni mwa wasanii wengi waliofaidi michano ya G Nako katika ngoma zao. Hawa wote wanafanya muziki unaoshabiana kwa kiasi kikuwa.
Rama Dee alimpa shavu G Nako kwenye wimbo uliofahamika kama ‘Make up’ chini ya prodyuza Pancho Latino wa B Hit’s. Kwa upande wa Damian Soul aliweza kumshirikisha G Nako katika wimbo wake uitwao ‘Tudumishe’ uliotoka chini ya studio za Legendary Music, tuachane na hilo.

Katika wimbo wa ‘Chizika Remix’ wa kundi la Fly But Ghetto (FBG) kutoka Arusha ambao G Nako na DJ Fetty walishirishwa, G Nako anasikika akipasuka ile mbaya katika verse ya kwanza.
Pia G Nako ameimba na kurap kwenye nyimbo kama’Laini’, ‘Show love’ ya Nako 2 Nako Soldiers, ‘Bum Kubum’ ya Nikki wa Pili, ‘Gere, Yakulevya na Dude’ zote za Weusi, na ile ‘Nisome’ aliyofanya na Godzilla.
Wenyewe athibitisha
Niliyoandika hapo juu yanathibitishwa na yeye wenyewe kwa kuangalia namna anavyokuwa akifanya katika nyimbo zake binafsi. Kuna baadhi ya nyimbo zake amewashirikisha wasanii wanaoimba, na nyingine wanaorap (hip hop).
Peter Msechu, Ben Paul, Jux na Belle 9 wapo katika orodha ya wale wasanii wanaoimba waliopata nafasi ya kusikika katika ngoma za G Nako. Peter Msechu alishirikishwa katika ngoma ya ‘Bado Ngware’, ambayo remix yake alimshirikisha Nikki wa Pili. Ben Paul alisikika katika wimbo wa ‘Mama Yeyo’ ulitoka mwaka 2013.
Chemistry yake na Belle 9 na Jux ni kitu kingine cha kumfanya kuendelea kuwa bora katika muziki wake. Kwa sasa yeye na Belle 9 wanafanya vizuri na wimbo wao mpya ‘Ma-Ole’ ambao G Nako ameonyesha uwezo mkubwa wa kuimba, hii ikiwa ni ngoma ya tatu kufanya pamoja baada ya remix ya Burger Movie Selfie na Give It To Me zote za belle 9.
Katika ngoma yake na Jux ‘Go Low’ ameonyesha uwezo na ubunifu wa kiwango cha juu katika Chorus na pia tumeona alivyochana katika Verse ya kwanza, hii ikiwa ni ngoma ya nne kukutana wawili hawa baada ya ngoma ‘Safari’ ya Nikki wa Pili, remix ya Burger Movie Selfie ya Belle 9 na ‘Hapo’ ya Quck Rock ambazo ameimba kidogo na kurap. Pia katika ngoma yake ‘Bado Muda Kidogo’ aliyofanya na Chindo Man na JCB ameonyesha uwezo wa kumudu vyote kwa wakati mmoja.
Wakati tukijiuliza imani ya G Nako ni ipi katika muziki huu, katika ngoma yake mpya ‘Luck Me’ aliyoimba mwanzo mwisho, ameonyesha imani yake ni kubwa kupitiliza katika muziki huu. unajua kivipi?.

Kitendo cha kujitolea kulala katika jeneza inaonyesha ni kwa kiasi gani anaamni katika sanaa yake na kuthubutu mambo ambayo hatujayazoea katika sanaa yetu, na ndio sababu ya wengi kuwa na maswali na mshtuko kuhusu kitendo hicho.
Alipoulizwa juu ya hilo G Nako alijibu “Watu wanaingia kwenye majeneza kila siku, watu wanauliwa kwenye movie kila siku, sio kitu kigeni sana ni kwa sababu tumechelewa kuingia kwenye tasnia ya muziki”.
Sasa kwa mchanganuo huo mfupi naweza kusema imani ya G Nako ni kubwa zaidi katika muziki wake, je imani hiyo ni katika rap au kuimba?. Naomba kuwasilisha.
Subscribe by Email
Follow Updates Articles from This Blog via Email

No Comments